Na Arone Mpanduka
Chimbuko la bendi ya Maquis du Zaire kwa nchi ya Tanzania lilianzia mwaka 1973, wakati Franco Luambo Luanzo Makiadi akiwa na bendi yake ya T.P. OK. Jazz alikuja hapa nchini na akafanya onyesho kamambe katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam(sasa uwanja wa Uhuru).
Mwaka mmoja baadae wa 1972, bendi ya Maquis du Zaire, nayo ikaingia kwa mbwembwe na kuweka makazi yake ya kudumu katika jiji la Dar es Salaam.
Bendi hiyo Maquis du Zaire iliyotokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ikafia humu nchini miaka ya 1990.
Ilikuwa kivutio kikubwa kwa Watanzania na kuwapa hekaheka wanamuziki wa Tanzania katika miaka hiyo.
Kwa nchini Congo, bendi hiyo ilianza mwaka 1960, vijana wa wakati huo katika mji wa Kamina huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), waliungana na kuunda bendi yao, wakaiita Super Theo.
Bendi hiyo ilikuwa ikitoa burudani tosha kwa wapenzi wa muziki wa mji huo wa Kamina na vitongoji vinavyouzunguka mji huo. Baadae wakaibadilisha majina na bendi ikawa Super Gabby. Lakini uongozi wa Super Gabby ulitaka kuleta mageuzi katika muziki mwaka 1972, walipobadilisha majina rasmi na kuwa Maquis du Zaire.
Mwaka huo huo bendi hiyo iliingia hapa Tanzania wakipitia nchini Uganda.
Walipofika katika jiji la Dar es Salaam, walipata mkataba wa kupiga muziki katika ukumbi wa Mikumi Tours, uliokuwa maeneo la Tazara Buguruni, jijini Dar es Salaam.
Baada ya kumaliza mkataba wao, waliondoka wakaenda kupiga muziki katika Klabu ya Hunters kwa kipindi kifupi.
Kisha viongozi wa bendi hiyo wakafanya mazungumzo na mfanyabiashara Hugo Kisima, aliyekuwa akimiliki ukumbi wa Safari Resort, maeneo ya Kimara, jijini Dar es Salaam. Wakaanza kupiga muziki kwa mkataba na mfanyabiashara huyo.
Februari 1977 viongozi wa bendi hiyo ya Maquis du Zaire, waliamua kukiongezea nguvu kikosi chao. Hivyo walimtuma Tchibangu Katayi ‘Mzee Paul’ aliyekuwa mwanamuziki wa bendi ya Maquis du Zaire.
Pia alikuwa mmoja kati ya viongozi wa bendi hiyo.Mzee Paul aliwachukua baadhi ya wanamuziki ili kuja nao Tanzania kuongeza nguvu katika bendi ya Maquis du Zaire.
‘Mzee Paul’ alibahatika kuwachukua wanamuziki akina Kikumbi Mwanza Mpango, au ‘King Kiki’, mtunzi na mwimbaji, Kanku Kelly kwa upande wa tarumbeta., Ilunga Banza ‘Mchafu’, aliyekuwa akiungurumisha gitaa la besi, Mutombo Sozy aliyekuwa akizicharanga ‘drums’, na mnenguaji Ngalula Tshiandanda.
Wakati huo Maquis du Zaire walikuwa wakicheza muziki wakitumia mtindo wa ‘Chakula Kapombe’, ambao kwa Watanzania ulikuwa mpya, na ukapendwa mno na mashabiki.
Kufika kwa wanamuziki hao, kulileta changamoto kubwa katika muziki. Tungo nzuri za Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’, zilikuwa chachu masikioni mwa wapenzi wa muziki wa dansi. Kiki pia yaelezwa kuwa ndiye aliyeleta Mapinduzi makubwa ya muziki hapa nchini Tanzania.
Maquis du Zaire wakaazisha mtindo mwingine wa ‘Kamanyola’, uliowapagaisha wapenzi na wadau toka pembe zote za jiji la Dar es Salaam.
Mwishoni mwa 1977, Marquis du Zaire walimaliza mkataba kwa Hugo Kisima, wakaondoka.Bahati nyingine ikawadondokea tena baada ya kuingia mkataba mwingine wa kupiga muziki kwa mzee Makao, aliyekuwa akimiliki ukumbi wa Savannah, maeneo ya Ubungo.Wakiwa Savannah, walianzisha mitindo ya ‘Sanifu’, na ‘Ogelea piga mbizi’.
Lakini ukumbi huo ukabadilishwa jina ukaitwa White House. Ikumbukwe kwamba Maquis pia ilikuwa ikipiga kwenye ukumbi wa Mpakani, maeneo ya Mwenge.Mwishoni mwa mwaka 1978, Maquis du Zaire waliamua kuimarisha tena kikosi chao kwa kuwaleta wanamuziki wengine wapya kutoka DRC.Iliwaleta akina Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe, Ngoyi Mubenga na Khatibu Iteyi Iteyi.
Bendi hiyo ilikuwa ikiongozwa na wanahisa akina Chinyama Chiyaza ‘Chichi’, Chibangu Katayi ‘Mzee Paul’, Chimbwiza Mbangu Nguza au ‘Nguza Vicking’, Mutombo Lufungula ‘Audax’ na Mbuya Makonga ‘Adios’.
Chini ya uongozi huo, katika miaka ya 1980 mafanikio makubwa yalionekana, mojawapo ni lile la kuanzisha Kampuni iliyofahamika kama Orchestra Maquis Company (OMACO).
Kampuni hiyo iliweza kumiliki shamba la matunda, wakalima kwa kutumia trekta zao maeneo ya Mbezi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Mazao yao walikuwa wakiyapeleka na kuuza katika Soko Kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam.OMACO pia ilimiliki mradi mwingine wa viwanja tisa na nyumba kadhaa, maeneo ya Sinza, jijini Dar es Salaam.
Kwa wakati huo, watu wengi hawakuwa na haja ya kuchukua teksi kurudi nyumbani, kwani muziki wa Maquis du Zaire ulikuwa unarindima hadi alfajiri. Muda ambao mabasi ya UDA ya Ikarus yalikuwa yameanza kazi. Wakati huo hazikuwepo ‘Dala dala’, Bajaji wala Pikipiki kwa maana ya Bodaboda.
Hata hivyo, baadae bendi hiyo ilianza kufa taratibu kufuatia baadhi ya wanamuziki kuondoka kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine, na wengine kusahindwa kufanya kazi hiyo kutokana na umri kuwa mkubwa, na magonjwa ya hapa na pale.
Mwanzoni mwa miaka ya 1990, bendi ilipotea kabisa na kuacha historia ya kipekee.
Baadhi ya nyimbo za Marquis du Zaire zilizovuma kwa uzuri na utamu wake ni ‘Ni Wewe Pekee; Makumbele; Kalubandika; na Promotion’.
This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.